REHEMA WA NJIA PANDA(03)


Miaka mitano baada ya kuanza kazi Anord alipatwa na ugonjwa wa ajabu.Ilikuwa Siku ya
jumamosi kama kawaida yake alikuwa na mazoea ya kufanya ziara za kushitukiza kwenye ofisi
zilizokuwa chini ya idara yake wilayani.Akiwa ndani ya gari la serikali ambalo lilitumika tangu
zama za ukoloni Anord alimwona mtu ambaye kama aliwahi kumwona mahali.
Akamwambia dereva wake asimamishe gari, kisha alishuka na kuelekea upande aliomwona yule
mwanamke.Baada ya hatua kama tatu macho yake yakakutana na mwanamke aliyekuwa
akimfuata akiwa amekaa chini ya mti wa maembe.
Alijikuta akishindwa kabisa kusogea, akajaribu kunyanyua mdomo wake aseme kitu lakini
mdomo wake nao ukawa mzito kutamka kitu .Wakabaki wakitazamana tuu bila kuongea
chochote.
Macho yao yalijaribu kuzungumza lakini nayo yalipoteza uwezo huo, kila alipojaribu
kumwongelesha kwa macho alishindwa.
Baada ya kuduwaa kwa takribani dakika mbili, hatimaye macho yao ama tuseme nafsi zao
zikazungumza.
“Njoo, mwenzako nateseka hapa"
“Mie siwezi mrembo wangu, njoo wewe"
“Mie siwezi nipo kifungoni"
"Kifungoni! Kakufunga nani? "
Waliendelea kujibishana kwa hisia huku kila mmoja akionekana kumhurumia mwenzake.
“Bosi si unaliona wingu twende barabara itachafuka" Sauti ya dereva wake ilimshtua Anord
ambaye ni kama alikuwa amerudishwa kwenye ulimwengu mwingine na kumfanya afikiche
macho kuhakikisha kama alikuwa akiota.Hakumwona yule binti aliyekuwa akiongea naye kwa
hisia bali watu wengi wakiendelea na shughuli zao za kila siku huku wakionekana kuchukua
tahadhari ya mvua iliyoonekana kutarajiwa kunyesha.
"Hivi nimetumia muda mrefu sana?" Aliuliza baada ya kuingia garini.
“Umemaliza dakika thelathini ukishangaa watu"
"Acha uongo wako wewe hata dakika tano hazijafika"
“Tano?, we kweli umechanganyikiwa" aliongea akiondoa gari.
“Nimechanganyikiwa, mpumbavu mkubwa wewe kwa hiyo bosi wako amechanganyikiwa?
Hembu nipishe hapa nimekuajiri upate kulisha familia yako nawe unajitia kidume kuniona
nimechanganyikiwa, toka mpumbavu wewe" aliongea Anord kwa hasira huku uso wake
ukibadilika na kuwa mwekundu.
Tangu aanze kufanya kazi kama dereva wa afisa manunuzi wa mkoa ule miaka minne iliyopita
hakuwahi kumwona bosi wake akiwa amefura kiasi kile huku akisifika kwa kuwa na utani
mwingi kwa wafanyakazi waliokuwa chini yake.Alimtania na kutaniwa na kila mtu bila kujali
nafasi yake au jinsi, mabinti walitania na kumaanisha kuhitaji ndoa naye lakini aliishia
kuwaambia ataoa Mbeya tena mke wa kutafutiwa na bibi yake.
Lakini kwa wakati ule alionekana kutokuwa Anord aliyezoeleka, dereva alitoka garini kuzuia
jambo lolote baya kumfika kutoka kwa bosi yule kinyonga aliyegeuka mbogo ghafla.
Baada ya dereva wake kushuka aliusogelea usukani akiwa na hasira na kutaka kuendesha gari
lakini alijikuta akilegea na kuangukia usukani jambo lilimfanya dereva wake aliyekuwa
akimwangalia arudi garini na kumwangalia bosi wake ambaye licha ya kumtimua garini muda
mfupi uliopita alikuwa akimwona kama ndugu yake wa damu tangu siku ya kwanza ambapo
alimchukua kwa shangazi yake miaka mitano iliyopita na kupeleka chuo cha ufundi Ifunda
alikojifunza Umakanika na udereva kisha kumwajiri kama dereva wake.
Aliingia garini na kujaribu kumwinua, Anord alijaribu kumzuia huku akijaribu kuzungumza kitu
lakini alionekana kuishiwa nguvu kabisa hata zile ndita zilizokuwa usoni lake zilikosa nguvu na
kuonesha sura iliyojaa unyonge.Alifanikiwa kumweka kwenye siti ya pembeni na kumfunga
mkanda kabla ya kuwasha gari kwa kasi ya ajabu kuelekea hospitali.
Alipofanikiwa kuiweka gari lile la kizamani barabarani sawasawa hakuwaza kitu kingine zaidi
ya kutaka kujaribu kuokoa maisha ya bosi wake.Akiwa katika kasi ya ajabu alishtuka kuona roli
la kampuni ya tumbaku ikiwa ipo katikati ya Barabara huku watu kadhaa wakihangaika
kufungua tairi la mbele, hakufanikiwa kufikiria kitu zaidi na kujikuta akijigonga kwenye kitu
kizito na giza totoro lilikamata macho yake.
Mafundi waliokuwa wakitengeneza Lori walipoona gari ikija kasi mahali walipokuwa
wamesimama waliamua kuyanusuru maisha yao kwa kukimbilia pembeni ambako waliamini
wangekuwa salama.
Kilichofuta wengi walishindwa kukisimulia japokuwa walikuwa wamekishuhudia kwa macho
yao mawili mazima bila hata kasoro yoyote.Kilichoshuhudiwa ni mwili mmoja kutolewa kupitia
kioo cha mbele cha gari kabla ya kutua juu ya lori na kutua chini ambapo mapande ya nyama
zenye damu yalionekana yakiwa yamesambazwa barabarani.
Gari liligonga lile lori na kutupwa pembeni na kama ilivyokuwa kawaida watu walilisogelea na
kuanza kuchungulia kilichokuwemo ndani mwake.
Hakuna aliyeamini alichokishuhudia ndani ya lile gari dogo na kumfanya kila aliyeona asogee
pembeni na kumtaka mwenzake aone alichokiona na kuhakikisha kama naye ataamini.
*****
Watu wote waliokuwa wamelizunguka lile gari huku wakishangaa kuona mtu ambaye alikuwa
kwenye ajali mbaya kama ile kusinzia ndani ya gari na kuota ndoto ambayo bila shaka na
ilikuwa ya mahaba kutokana na jinsi alivyokuwa akifanya kabla ya kujibamiza kwenye Chuma
kilichokuwa kimechomoza na kumsababishia jeraha kubwa lililokuwa likitoa damu nyingi sana
na kurukia nje .Walimtoa mtu yule na kumpa huduma ya kwanza kuzuia damu kutoka kisha  kumpakia kwenye gari lingine lililokuwa limesima baada ya njia kuzibwa na magari yaliyokuwa
yamepata ajali.
Anord licha ya kuwa na jeraha kubwa lililokuwa likimtisha kila mmoja aliyeliona hakusikia
maumivu yoyote huku akikumbuka ndoto aliyokuwa akiiota.Alimkumbuka Sikujua lakini
aligundua Sikujua yule alikuwa na nywele ndefu na mweusi zaidi ya Sikujua aliyekuwa
akimfahamu.Lakini zaidi alikumbuka kuwa Sikujua alikuwa ameolewa huko Dodoma miaka
miwili ikiyopita na ni yeye ndiye aliyempeleka stesheni ili akapande treni.
''Hapana !'' Anord alijikuta akiongea kwa sauti kubwa na kuwashtua wauguzi waliokuwa
wamembeba kwenye machela kumwingiza wodini.
Baadaye aliamua kulala tena baada ya kugundua kuwa kushtuka kwake kuliifanya damu iendelee
kutoka kichwani pake.Ndani ya wodi madaktari waliendelea kuhangaika kuokoa maisha yake
lakini akili ya Anord ilikuwa ikimfikiria mrembo ambaye alikuwa amempa raha
usingizini.Hakutaka kabisa kufanya kitu kingine zaidi ya kutaka kupata utamu ambao Sikujua wa
usingizini alikuwa akiendelea kumpatia.
Masaa kadhaa ya kusafisha na kushona jeraha lililokuwa kichwani kwa Anord alijaribu kurejesha
kumbukumbu kichwani mwake na kurejesha akili hiyo kwenye ulimwengu wa kawaida ,
alikumbuka tangu alipomwona msichana mrembo ambaye walijibishana kwa macho ,ugomvi na
dereva wake na kisha kumfukuza.Akili yake ilimkumbusha pia chanzo cha ugomvi wao,
ambacho alijua kabisa kuwa hakuwa sababu ya kumfukuza ndugu yake ambaye alikuwa
ameenda kumchukua kijiji kwao.Hakujua kabisa kuwa ndugu yake huyo ambaye ndiye dereva
wake aliyekuwa amemfukuza masaa machache yaliyopita hakuwa tena hapa duniani bali alikuwa
ameshafariki.
Akili yake haikumwambia kuwa aliyekuwa akiendesha gari alikuwa si yeye bali dereva wake
aliyekuwa amefariki.
Alifikiria mahali ambako ndugu yake huyo angekuwa, alijua kabisa alikuwa amemsababishia
mateso bila sababu yoyote ikizingatiwa kuwa alikuwa ugenini ambako kwa haraka haraka
suluhisho lingekuwa ni kushinda kwenye mashamba ya tumbaku kufanya kazi jambo ambalo
hakutaka kabisa litokee.
Majira ya saba mchana gari la serikali lilifika hispitalini na kumchuka kwani alikuwa si mtu wa
kulazwa huku mwenyewe akiwa hana maumivu yoyote zaidi ya kutishwa na wingi wa damu
iliyokuwa imemwagika.
''Pole kwa msiba ndugu yangu'' Aliongea dereva aliyekuwa akiendesha gari walilokuwa
wamepanda baada ya kumfikisha nyumbani kwake.
''Msiba nani amekufa?"
“Dereva wako mlipopata ajari alipoteza maisha pale pale''
Anord alijikuta akishindwa kujizuia taratibu machozi yalimshuka na akajikuta akikaa chini pale
pale mlangoni.Hapo ndipo kumbukumbu kuwa alikosa nguvu mara tuu alipotaka kuendesha
gari.Aligundua kuwa dereva wake ndiye aliyekuwa anaendesha gari pia taswira ya tukio la
kuchomwa na chuma ndani ya gari ilijirudia kichwani kwake alijiona akiwa kwenye kiti cha
pembeni huku nyama na damu zikiwa zimesambaa ndani na nje ya gari.Alijilaumu sana kwa
kitendo chake cha kugombana na dereva wake kwani alihisi kuwa kumgombeza kulimfanya
aendeshe gari huku akiwa na mawazo hatimaye alikosa umakini kabla ya kupata ajali hiyo.
Hayo yote yalipita akilini mwake haraka haraka sana akiwa palepale chini mlangoni.
Alisaidiwa kuingia ndani na yule dereva aliyemleta kabla ya kuja wafanyakazi wenzake
waliokuja kuandaa mazingira ya msiba kwani marehemu alikuwa akiishi naye kabla mauti
kumfika na yeye pekee ndiye aliyekuwa ndugu pale Tabora mjini ndugu wengine walikuwa
Sumbawanga ,Kigoma na Dodoma wengi walikuwa Mbeya na kwa njinsi mwili wake
ulivyokuwa umeharibiwa isingewezekana kuusafirisha hadi Mbeya.itaendelea

Comments

Popular posts from this blog