GEREZA LA GITARAMA: Jehenamu duniani!



By @BIN CYPHER
Jiji la Gitarama hupatikana katikati ya nchi ya Rwanda, kwa makadirio kilomita arobaini na tano toka kwenye jiji kubwa nchini humo; jiji la Kigali, jiji pekee lililoitangulia Gitarama kwa ukubwa.
Kama haitoshi ni hapahapa katika jiji hili ndipo kuna historia kubwa ya makutano yaliyofanyika mwezi wa kwanza; mwaka 1961, Rwanda ikatangazwa rasmi kama jamhuri. Vilevile jiji hili (kipindi hicho mji) likatoa raisi wa kwanza wa Rwanda, bwana Gregoire Kayibanda, ambaye kumbukumbuye mpaka sasa imesimamishwa katikati ya eneo hili.
Mazuri hayo hayakomei hapo, hapana! Bali pia hili jiji likabarikiwa na kutunukiwa vivutio kadha wa kadha vya utalii na taasisi lukuki za elimu ambazo aidha zaweza jaza ukumbi nikizianisha hapa. Na kwa namna moja ama nyingine nachelea kusema taasisi hizo zilijengwa (zimejengwa) kwa lengo chanya la kuwafanya watu wapate elimu na hatimaye kujikomboa kifikra na kimwili.
Lakini mbali na taasisi hizo, na aidha vivutio na uzuri wa jiji hili, upande wa pili wa sarafu ukisikia jina hili ‘Gitarama’, yakupasa uhofie na hata kushikwa na huruma kwa namna binadamu kama wewe wanavyotendwa, tena bado wakiwa hai kabisa. Binadamu hao wakiwa wanaishi ndani ya eneo ambalo hakuna binadamu yeyote juu ya uso wa dunia angelipenda kuwamo kwa gharama yoyote ile!
GITARAMA; ‘JEHANAMU DUNIANI’:
Sehemu nyingi duniani zimewahi kuitwa jehanamu. Na jina hili lilishamiri zaidi baada ya vita vya pili vya dunia ambapo maeneo kadhaa yalipewa jina hili kuwakilisha maeneo yasiyokalika, hatari na yasiyo na afya stahiki kwa wanadamu. Maeneo hayo mathalani ni Blood Falls (Maanguko ya damu) huko Antarktika, Danakil Depression (bonde la Danakil) huko Ethiopia, Door to Hell (mlango wa kuzimu) huko Turkmenistan, Kamchatka Peninsula huko Russia na kadhalika, na kadhalika.
Japokuwa sehemu hizo zipo nyingi zikipatikana maeneo mbalimbali, ni dhahiri kuna sifa ambazo hushirikiana na hivyo basi ndio maana huwekwa chini ya mwamvuli mmoja wa ‘jehanamu’.
Upande wa kusini magharibi mwa jiji la Kigali, ndipo ilipo jela hii Gitarama. Kwa sasa inaitwa jela ya Muhanga ikichukua jina la wilaya ambayo ndiyo makazi yake mpaka sasa. Majengo ya jela hiyo yalikuwa yanamilikiwa na waingereza British housing complex mnamo mwaka 1960 yakiwa yamejengwa kama makazi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Pale kampuni ilipofungwa, eneo hilo likakodiwa na serikali ya kwanza ya Rwanda iliyokuwa imedhamiria kufanya majengo hayo kuwa jela ya kisiasa (political prison). Tangu hapo hakuna chochote kilichobadilika ndani ya jela hiyo isipokuwa tu serikali ya Rwanda ambapo kila serikali iliyoingia madarakani ilionekana kuipatia ama kuitafutia matumizi eneo hilo.
Kwa mujibu wa gazeti la London Independent mwaka 1995, hii ndiyo jela mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani. Pia wanda za tovuti nyingi za mitandao, zinakiri na kuiweka jela hii kwenye kumi, ama tano, ama tatu bora zaidi ya jela hatari mno kuwahi kutokea duniani.
Gitarama ilijengwa kwa ajili ya kumudu wafungwa mia nne tu, lakini mpaka sasa inabebelea wafungwa elfu saba! Mara kumi na nane kwa makadirio. Hali hii inapelekea mahesabu ya wafungwa wanne kurundikana katika eneo la hatua tatu (three feet). Hili laweza likawa la kawaida sana ukilisoma hapa, lakini ukijaribu kutoka nje ya bandiko hili na kujikuta ukiwa umekaa na watu wengine watatu ndani ya eneo la hatua tatu tu, kidogo waweza kuelewa.
Hakuna mahali pa kulala, kujilaza, wala pa kuketi. Wafungwa husimama wakikung’utwa na jua na wakipoozwa na mvua kwakuwa jela hii kwa kiasi kikubwa haina paa la kuwakinga wafungwa na jua, mvua wala baridi.
Kutokana na kutapakaa kwa wafungwa hao kwenye eneo hilo dogo, inakuwa ngumu sana kwa mfungwa kutaka kwenda chooni akafanikiwa kwa muda, hali hii inapelekea wafungwa kujisaidia popote pale na hivyo basi kujaza vinyesi, mikojo na harufu kila eneo. Wafungwa huozeshwa na kumomonywa miili na bakteria mpaka kufa kwasababu ya kujiweka karibu, aidha kwa kulala ama kusimama kwenye vinyesi na uchafu wa kila aina (gangrene).
Wafungwa wengi hawana vidole, nyayo na miguu kwasababu ya kuoza wakiwa hai. Miguu hubadilika rangi na hata kutoa madonda. Ni kawaida kuona mtu ana wadudu miguuni huku wakitembea.
Kati ya wafungwa kumi ndani ya jela hii, nane hufa kwa kukosa hewa ama magonjwa mbalimbali. Lakini wanapotoka kwenda kuzikwa, basi huingizwa wafungwa wengine ndani ya mlango mkubwa wenye kutu wenye kutoa malalamiko ya ukuukuu.
Lakini ajabu na kweli ni kwamba, wafungwa waliomo humo ndani hakuna hata mmoja ambaye amepitia mahakamani akathibitishwa ya kwamba ana makosa na anastahili kufungwa.
Wengi wao, kama si wote, ni wa Hutu. Na walianza kujazwa humo miaka ya 1990's wakituhumiwa kwa mauaji ya Kimbari yaliyokwapua maisha ya wana Rwanda zaidi ya milioni moja. Na hii huonekana ni sababu kubwa inayofanya serikali kutokujali kabisa jela hiyo achilia mbali aliye madarakani ni mtutsi.
"Watu wanafanyana vitoweo."
Si tu kwamba hakuna mahali pa kupumzikia, bali ndani ya jela hii kuna rekodi kadha wa kadha mfungwa kumuua mwenzake kisha kumla kama chakula.
Mgawo wa chakula ni finyu sana. chakula na maji hutolewa mara moja tu kwa juma, tena kikiwa kibovu na hakitoshelezi; mara nyingine chakula kinakosekana kabisa na hivyo basi kuwalazimu wafungwa kumaliza siku kadha wa kadha pasipo kutia kitu tumboni.
Kwakuwa kila mtu anataka kuishi, wafungwa wengine huamua kuchukua hatua ya kulinda uhai wao kwa kuwanyonga wenzao, kuwabamiza ukutani mpaka mauti kisha kuwatafuna wakiwa wabichi na wakivuja damu moto.
Wengine hucheza kamari kabisa, ambapo wahusika huchaguliwa kwa kukurupushwa. Mwisho wa siku wahanga wa Kamari hiyo hupotea isijulikane wameenda wapi ndani ya jela, bali matumboni.
Kumbuka kwamba yote haya yanawezekana tena kwa urahisi kwa sababu ndani ya jela hii hakuna hata mlinzi anayediriki kuingia, ni wafungwa wenyewe tu ndio ambao hujihudumia wenyewe. Chakula na maji vikiletwa, huachwa mlangoni kabla ya wafungwa wenyewe kunyakuwa na kuanza kujigawia. Ndio maana mtu anaweza akafa mpaka akaoza ndani ya jela hii kabla hajaja tolewa na kwenda kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja.
Kulana wenyewe kwa wenyewe si jambo geni wala la kushhtukiza kwa walinzi wa jela hiyo wala tawala husika.
Juhudi za kubadilisha hali ya Gitarama:
Kwa namna moja ama nyingine kuna watu na mashirika yaliyoguswa na hali ya kusikitisha kuhusu Gitarama. Japokuwa kweli waliomo humo wanaweza wakawa ni watu waliofanya makosa mbalimbali, ikiwemo hata kuua, lakini halibadilishi dhana ya kwamba na wao wanahitaji haki za binadamu kama wengineo.
Shirika la Global Giving, likisukumwa na kiongozi wa projekti hii Karen Tse, ni moja ya shirika lisilonuwia faida lililoguswa na hata kuanzisha kampeni ya kutafuta pesa kwa ajili ya kuwasaidia wafungwa hao. Mpaka sasa shirika hili li wazi na unaweza ukawachangia.
Pesa waliyoichangisha mpaka sasa ni dola za kimarekani 325 huku wakifadhiliwa na mashirika mawili fadhili na huu ukiwa ni mwaka wa sita sasa wapo moto (active).
Mbali na hapo wanajitutumua kuwasaidia wafungwa hao kisheria ili kesi zao zipatwe kusikilizwa mahakamani. Japokuwa swala hili linaonekana ndoto zaidi ya uhalisia tangu mkono wa serikali unakuwa mzito sana kutingisha kidole.
“Hiyo ndiyo Gitarama; jehanamu juu ya uso wa dunia. Ama tuseme tawi dogo la jehanamu duniani.”

Comments

Popular posts from this blog