MZIGO(SEHEMU YA 1 & 2)

Niliwasili Dar es salaam saa tisa na nusu
alasiri. Hii ilikuwa ni mapema zaidi
kuliko nilivyotarajia. Safari yetu ilichukua
siku tatu. Watu walikuwa wametawanyika ovyo pale
kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo. Walikuwa kama
siafu walioangukiwa na kaa la moto. Miongoni mwao
walikuwa ni abiria ambao wanasafiri huku wengine
wakiwasili. Pia walikuwepo wapiga debe ambao
walileta kero kubwa kwa abiria.
Bonge alinionya kuwa nisipitie sehemu nyingine
kabla ya kumfikishia mzigo wake. Pia alinionya kuwa
iwapo sitatekeleza maagizo yake, basi asingenipa
malipo yangu kwa kazi ya kusafirisha mzigo ule. Vile
vile alinikumbusha kuhusu ile picha ya hatari. Ni picha
yangu ambayo ilikuwa inaniweka katika wakati
mgumu. Ni picha ambayo leo inanifanya niwe mtumwa.
Kwa sababu ambazo mpaka leo sijazielewa
nikaamua kuvunja maagizo yake kwa kupitia nyumbani
kwangu Yombo Buza. Sifahamu kama kuna nguvu ya
ziada kutoka nje ya nafsi yangu ilinituma kufanya
uamuzi huo wa aina yake; Kuvunja maagizo ya mtu
kama Bonge halikuwa jambo la kawaida.
Ilikuwa siku ya tatu toka nikabidhiwe begi lile.
Sikujua kilichomo ndani yake ingawa hisia zilinituma
kuwa huenda ni almasi. Kidogo nikaanza kuingiwa na
mashaka kwani nilionywa kuwa iwapo nitathubutu
kufungua tu, basi adhabu yangu itakuwa ni kifo! “Hivi
kweli nikiufikisha huu mzigo nitaweza kuepukana na ;hicho kifo?” Lilikuwa ni swali gumu ambalo nilijiuliza
bila kupata majibu.
Lazima nifungue kwani Martin na Bonge watajuaje
kuwa mzigo umefunguliwa?
Nilipofika chumbani nikalitua begi lile kitandani.
Moyo ulikuwa unaenda mbio kama mtoto aliyemuona
daktari akiwa na sindano mkononi. Nilimfikiria sana
Martin. Huyu ndiye aliyenitisha zaidi, jinsi alivyo! Ana
umbo kubwa lenye misuli iliyojengeka kama mnyanyua
vitu vizito, macho yake ni makubwa kama kurunzi
huku uso wake ukipambwa na kovu kubwa lililopita
katikati ya uso wake. Kwa jinsi alivyo alitosha kabisa
kumnyamazisha mtoto anaelia kwa neno moja, huyo
Martin anakuja!
Pale alipokuwa ananitizama nilikuwa sijamkosea
chochote lakini alikuwa anatisha kama nyoka anayetaka
kumrukia mtu. Macho yake yalionyesha wazi dalili zote
za mtu mwovu kama si muuaji kamili. Atanifanya nini
akigundua kuwa nimefungua ule mzigo? Iwapo alikuwa
ananitazama kwa sura ambayo kwake ilikuwa ya upole
lakini nilibanwa na haja ndogo, vipi nikutane naye siku
ambayo amekasirika? Ndo ajue sasa maagizo
waliyonipa nimeyavunja, atanifanya nini?
Bila shaka atanifanya kama alivyofanyiwa yule
mwanamke kule guest. Sijawahi kuona mtu
aliyeuwawa. Maiti ambazo nimewahi kuziona kwa
macho yangu ni za ajali ya gari. Taswira yake ilinijia
kichwani mara kwa mara. Mwili ulisisimka na kufanya
vipele vidogovidogo kama mtu anayehisi baridi kali.
Maskini Merina, Mungu amlaze mahali pema peponi.
Amin.
Shauku yangu ya kutaka kujua kuhusu mzigo
ule ilisababishwa na vitisho vya Martin na Bonge.
Adhabu ya kifo kwa kufungua mzigo tu! Balaa
Laiti wasingenionya kiasi kile basi nisingekuwa na
wazo lolote juu ya mzigo ule. Ningeufikisha kama walivyotarajia bila hata kuwa na chembe ya wazo juu ya
mzigo wao.
Nikalikazia macho begi lile jeusi. Lilikuwa kama refarii
katika maisha yangu. Nifungue niishi kwa mashaka au
niache niishi kwa amani.
Kitu kimoja ambacho kilinikosesha raha ni kuwa iwapo
sitafungua basi nitakuwa na fumbo moyoni, fumbo
ambalo sitaweza kulifumbua maisha yangu yote.
Nakumbuka hata nilipokuwa mwanafunzi niliumiza
sana kichwa kwenye mafumbo. Nilikuwa sikubali
kushindwa. Kwa mara ya kwanza leo nakabiliana na
fumbo, fumbo ambalo kufumbua kwake ni kifo.
Nikubali kushindwa? Kweli nilikuwa naelekea
kushindwa. Lakini kwa nini nishindwe!?
Nikiwa mtaalamu wa mafumbo nilikuwa na kazi
mbili, kwanza mzigo halafu uhai wangu. Lengo lilikuwa
ni kujua kuhusu ule mzigo bila kupata matatizo.
Nikatabasamu huku nikiwa nalitazama vizuri
begi lile ambalo niliahidiwa pesa nyingi kwa kulifikisha
kwa muhusika bila kuvunja masharti. Fedha nilizo
ahidiwa sijawahi kufikiria hata siku moja kuwa nitakuja
nizitie mikononi.
Kwanini kulisafirisha lile begi kutoka Mwanza
nilipwe pesa zote hizo? Kutatua fumbo lile kwangu
lilikuwa jambo kubwa kuliko zawadi ambayo
ningepewa na bonge huku fumbo likiendelea kubaki
kama maisha ya kaburini ambayo maiti tu ndiye
anayejua yalivyo. Haiwezekani! Lazima begi lifunguliwe.
Kabla sijafungua nikapata wazo. Nikatabasamu.
Lilikuwa wazo kabambe. Nilitaka niue ndege wawili
kwa jiwe moja. Nilidhamiria kulifumbua fumbo lile bila
kuniletea matatizo. Nilianza kujihisi kuwa mshindi
ingawa bado niliendelea kujionya juu ya hatari ambayo Nilikua naanza kukabiliana nayo.�....itaendelea,KWA MAONI LIKE PAGE YETU FACEBOOK,KISHA TUTUMIE UJUMBE

Comments

Popular posts from this blog