MZIGO SEHEMU YA (3&4)

Kabla sijafungua nikapata wazo. Nikatabasamu.
Lilikuwa wazo kabambe. Nilitaka niue ndege wawili
kwa jiwe moja. Nilidhamiria kulifumbua fumbo lile bila
kuniletea matatizo. Nilianza kujihisi kuwa mshindi
ingawa bado niliendelea kujionya juu ya hatari ambayo
nakabiliana nayo.juu ya mambo ya ajabu ambayo yanatokea katika
maisha yangu.
ENDELEA.....
Muda huu mfupi ambao nilikaa hapo uliweza
kunifanya niyatazame maisha yangu kama mtu
anayetazama filamu ndefu ya kusisimua. Nilikuwa
kama mtu ninayejitazama mwenyewe kwenye kioo.
Ilikuwa kana kwamba ninajisimulia kitu fulani.
Naitwa Kajuna Daudi Kazakamba, ni mtoto wa
kwanza katika familia yenye watoto watatu, mimi na
wadogo zangu wawili wa kike Maua na Waridi………
***
Baadhi ya watu wanaoishi Dar es salaam wana
akili za ajabu na zinazofanana sana. Hawapendi kuishi
maeneo yenye nafasi na hewa nzuri. Hupenda sehemu
zenye misongamano ya watu na hususani zile zilizoko
kando ya barabara. Mfano mzuri maeneo kama
Kinondoni na Manzese. Hilo ndilo jambo lililomfanya
baba yangu kununua kiwanja eneo ambalo liko karibu
na barabara. Madhara yake yalikuwa makubwa kwa
baba na familia kwa ujumla.
Ikiwa ni miaka kumi na mitano toka ajenge
nyumba hiyo akapokea barua kutoka serikalini ikimtaka
kuhama eneo hilo. Katika barua hiyo serikali ilidai kuwa
baba amejenga katika eneo ambalo linatambuliwa
kisheria kuwa ni barabara. Nyumba yetu ikabomolewa.
Hakuna fidia iliyotolewa ingawa vyombo vya habari
vikiwanukuu viongozi husika vilitoa taarifa kuwa
waathirika wote wamepata fidia zao.
Ukawa mwanzo mpya wa maisha ya kupanga na
kuhamahama, mpaka pale baba alipojenga nyumba
nyingine Mwananyamala baada ya kupata fedha zake za
mafao kutoka shirika la reli Tanzania ambako alifanyia
kazi.
Fedha zote za kiinua mgongo ziliishia kwenye
ujenzi wa nyumba hiyo. Mwaka huo nilikuwa kidato
cha sita shule ya sekondari Tambaza. Mapema mwaka uliofuata nikahitimu masomo yangu. Kama zilivyo
hadithi za watoto wengine wanaotoka kwenye familia
kama zetu hapo ndio ikawa tamati sikuweza kuendelea.
Nikaanza kutangatanga kutafuta maisha.
Nikahama Mwananyamala kwa wazazi wangu
nikahamia Yombo Buza. Huko nilihama nyumba
kadhaa hatimaye nikapata sehemu ambayo nilikaa
muda mrefu kuliko nyumba nyingine.
Chumba kimoja, kitanda, ndoo na vyombo
vingine vilikuwa vinaonyesha taswira halisi ya maisha
yangu. Vilikuwa vimekusanyika pamoja, Hakukuwa na
tofauti kubwa na sehemu inayouziwa pombe za
kienyeji. Niliridhika kuishi maisha hayo kuliko
kumuongezea baba mzigo. Kwani biashara yake kubwa
kipindi hicho ilikuwa ni samaki ambao alikuwa
anawauza katika mitaa ya Mwananyamala na
Kinondoni.
***
Ilikuwa saa 12.30 jioni. Nilivua sare zangu za kazi
nikazitia kwenye boksi. Nikachagua nguo safi kutoka
kwenye kamba ya nguo. Kamba hiyo niliifunga kwenye
misumari ambayo niliigongea ukutani. Baadhi ya wenye
nyumba hawapendi mtindo huu wa kutoboa hovyo
nyumba zao kwa misumari. Nyumba niliyoishi haikuwa
na masharti kama hayo, vyumba vyote vilikuwa
vimetobolewa kwa misumari. Kimsingi ulikuwa ni
uharibifu ndio maana baadhi ya wenye nyumba
walikuwa hawaridhishwi na hilo. Sisi tulikuwa na
bahati kwani mwenye nyumba alikuwa mlevi hivyo
wewe fanya lolote lakini siku ikifika mpe chake akalewe.
Niliitazama kalenda ya kampuni ambayo
nilikuwa nafanyia kazi, nikagundua kuwa ilikuwa ni ya
miaka miwili iliyopita. Niliziangalia kwa hasira picha za
watu ambao walikuwa wanacheka kwenye kalenda ile.
Walikuwa na matumbo makubwa ambayo bila shaka
yalikuwa yamewazidi uwezo. Hivi hawa wanakumbuka
kweli kuwa kuna watu wanapata shida duniani au wanajali matumbo yao tu? Kwenye picha ile kulikuwa
na Watanzania wenye asili ya kiasia (wahindi) na wale
weusi kama sisi.
Nikaitazama tena kwa uchungu kalenda ile.
Kalenda mpya zilikuwa zinatoka kila mwaka, ili uweze
kupata kalenda hizo ulitakiwa kuwabembeleza waajiri
waweze kukupatia. Wengi wao walikuwa ni watu
wenye majivuno. Sikuwa na muda wa kumbembeleza
mtu. Kazi yenyewe sikuipenda, tatizo kubwa sikuwa na
kazi nyingine ya kufanya. Kilichonikera zaidi kazi
zenyewe hazikuwa za kila siku.
Tulikuwa tunarushiwa vikaratasi ambavyo
vimekunjwa, ukifungua unakuta idadi ya siku
utakazofanya kazi kwa mwezi pamoja na malipo
utakayolipwa. Ilikuwa ni kampuni inayojishughulisha
na utengenezaji wa juisi za aina mbalimbali, biskuti na
mikate. Ilikuwa ni miongoni mwa makampuni
yanayosifika sana kwa kusamehewa kodi. Nilipata
kusikia tetesi kuwa eti ni ya shemeji yake kigogo
mkubwa wa wizara nyeti. Roho iliniuma sana. Mungu
ametuzawadia sote hii nchi, lakini kuna watu
wanaoifanya kuwa mali yao. Hawa ni wale ambao hata
sheria haifanyi kazi upande wao.
Nilizikagua tena zile nguo nikaridhika kuwa ni
safi. Nilivaa shati jeupe, suruali nyeusi na viatu vyeusi.
Sikusahau kufunga tai siku hiyo. Nikaonekana kama
mmoja wa wafanyakazi wa benki kwa nguo
nilizozinunua kwa mmachinga. Nikazikagua nywele
zangu, hazikuhitaji kitana kuzichana. Nikachukua
brashi, nikaanza kupitisha kwenye nywele zangu ndogo
huku nikijiangalia kwenye kioo kidogo.�
Itaendelea....PERUZI KURASA ZA NYUMA ILI USOME KUANZIA MWANZO WA KISA HIKI
by author:-Bin cypher

Comments

Popular posts from this blog